HIVI NDIVYO “Sukuma Flavour” INAVYOICHINJA NA KUIZIKA “Bongo Flavour!” “Uwe na Pesa Matatizo,Usiwe na Pesa Matatizo!

 


HIVI NDIVYO “Sukuma Flavour” INAVYOICHINJA NA KUIZIKA “Bongo Flavour!”  

Uwe na Pesa Matatizo,Usiwe na Pesa Matatizo!” Maneno ya msanii wa Sukuma Flavour aitwaye Bhudagala Ng’wana Malonja.

Na:Prince Ngeni Mashamba.      

               Awali ya yote nitumie fursa hii kumshukuru Mungu mwenye enzi na mamlaka yote kwa upendeleo wa afya njema,matumaini na kesho yenye matumaini angavu-Utukufu wote kwa Mungu! Ni matumaini yangu kuwa,hata ninyi wapenzi wasomaji wa Makala zangu mko poa!

              Katika Makala ya leo nitakuwa nikiudurusu kwa mawanda mapana muziki wa Kitanzania maarufu saana kwa Ukanda wa Ziwa Viktoria ambao binafsi nimeupa jina la “Sukuma Flavour” kwa jinsi ambavyo unazidi kuziteka hisia za Watanzania wanaokimanya vyema Kisukuma.

             Mwaka 2021 mwezi wa Mei niliposafiri kutoka Daresalaam kwenda Kahama ikiwa ni mwaliko maalum wa Mkurugenzi wa shule nzuri sana ya Goodhope Secondary School iliyopo maeneo ya Mwendakulima katika kijiji cha Mondo;ndugu yangu Tajiri mtoto Frank Ernest,ninakumbuka baaada ya kufika Kahama na kama ilivyo kawaida ya ukarimu wa Watanzania hawa wa Kanda ya Ziwa,baada ya kunywa chai nzito sana iliyosindikizwa na samaki aina ya Sato;aliniwekea wimbo wa Msanii Ng’wana Kang’wa almaarufu Ntemi wa Mabala uitwao “Gonye.”

           Baada ya goma hilo kuanzwa kutwangwa kwenye kinu chake cha bei kali aina ya Sony,boss mtoto aliniambia,”hebu mtazame huyu msanii wetu ambaye sisi huku Kanda ya Ziwa tunamwona kuwa ndiye Diamond wetu!”

          Nilicheka tu na kimoyomoyo nikajisemea huyu boss wa Goodhope Secondary School huenda hamfahamu vizuri Chibu-Dii Chibu-Dee a.k.a Simba wa pori la Tandale yaani Diamond Platinumz kwa jinsi ambavyo hulishambulia jukwaa kwa ujuzi na usongo wa hali ya juu.

         Lakini mwaka 2024 niliposafiri kikazi kwenda Runzewe huko Kanda ya Ziwa,nilianza kuyakumbuka maneno ya mkurugenzi kijana kuliko wote Afrika ndugu yangu Frank Ernest baada ya kufika kwenye Bar nyingi za mjini humo zikicheza nyimbo za akina Kang’wa na wateja hawakuwa tayari kucheka na msanii “wowote” zaidi ya akina Kang’wa na wenzake akina Bhudagala,Gude Gude,Rogeti,Limbu Luchagula,Mayiku Sayi,Magodi Ze Don,Bugalama na wengine wengi ambao siwezi kuwataja wote kwa majina.

         Kwa ufupi tu ni kwamba,kwa sasa BongoFlavour haina chake kwenye Ukanda wote wa Ziwa Viktoria kwani Sukuma Flavour imeshika hatamu balaa! Nilipojaribu kufanya utafiti wa kwa nini Sukuma Flavour imeliteka soko la muziki na hisia za WanaKanda ya Ziwa,haya hapa ndiyo niliyoyabaini kama nitakavyoyadadavua hapa chini.

         

          UJUMBE UNAOGUSA MAISHA HALISI YA WATANZANIA:-Tofauti ya jumbe za Bongo Flavour ambazo nyingi zimechakachuliwa yaani hazieleweki kama ni za Kitanzania au kutoka nje,Sukuma Flavour jumbe zao zinatokana na maisha halisi ya Kitanzania yaani wanaimba yaliyomo kwenye jamii ya Watanzania wenyewe.

          Hili linathibitishwa na wimbo kama “ILANGE yaani Maadili” ulioimbwa kwa ushirikiano kati ya Rogeti na GudeGude.Wimbo huu unaelezea jinsi gani mwingiliano wa tamaduni za nje na kukua kwa Sayansi na Teknolojia kulivyochangia kuporomosha maadili ya Kitanzania na Waafrika kwa ujumla.Nyumbani watu wote wana ndevu,haijulikani nani ni Baba na nani ni mama wala nani ni mtoto.

        Nyimbo nyingine zenye ujumbe unaogusa maisha ya kila siku ya Watanzania ni kama vile “ICHOLA” ulioimbwa kwa ushirikiano kati ya Rogeti na GudeGude,mizigo yote hiyo unaweza kuipata kwa uzuri zaidi kwenye YouTube channel.

         

         DRESSING CODE(MAVAZI YA HESHIMA):-Tofauti na nyimbo za Bongo Flavour ambazo ni ngumu sana kutazama video zake ukiwa na wazazi au wakwe zako;kwa upande wa Sukuma Flavour “manyalali wao yaani madansa wa Sukuma Flavour”;huvaa mavazi ambayo kwa sehemu kubwa yanazingatia maadili yetu ya Kitanzania.

        Hili linathibitishwa na nyimbo kama “SARAH na ZILIPENDWA” zilizoimbwa na msanii mwenye malofu mengi aitwaye Limbu Luchagula a.k.a The Boss.Ukitaka kuzifaidi nymbo hizi,ingia YouTube channel kwa raha zako zaidi.

       

        KUTANGAZA UTAMADUNI WETU:-Kingine kinachovutia zaidi kuwasikiliza na kuwatazama Wasukuma Flavour hawa ni mavazi yao yanayotangaza utamaduni na raslimali asili zilizopo nchini kwetu.Kwa mfano ukiutazama wimbo wa “NALI NSUKUMA” wa Ntemi Omabala Ng’wana Kang’wa;msanii huyu ametumia mavazi ya asili ambayo kwa kweli yanavutia sana kuyatazama-kongole kwake!

       Hali kadhalika,msanii Limbu Luchagula na pacha wake Sayi Mayiku,mavazi yao ni yale yavaliwayo na Wafugaji wa Kisukuma yaani “Bhademi!”  

       A.K.A.  ZAO SASA UTACHOKA!:-Ukiachilia mbali kutunga nyimbo zenye uhalisia wa maisha ya Kitanzania,wasanii hawa pia kwa mbwembwe hawako nyuma kama walivyo wasanii wengine.Na wao wamejipa majina ya kibiashara kila mtu kwa jinisi anavyoona inampendeza.

      Wakati Rogeti mzee wa Taarabu ya Kisukuma akijiita “A greatest song writer”;GudeGude yeye anajiita “Tagili omaluho” wakati huo huo Kisima Nyanda Majabala yeye hupenda kujiita “A greatest Singer!” Lakini Diamond wa Wasukuma yaani Ng’wana Kang’wa yeye hupenda kujiita “Ntemi Omabala!”

        CLOUDS MEDIA GROUP MNAFELI WAPI!?-Kwa kuwa binafsi ninaamini kabisa kuwa,mojawapo ya chombo cha habari chenye vijana wabunifu na wanaoijua vyema kazi yao ya Habari ni Clouds Media Group chini ya mkurugenzi Joseph Kusaga;niwaombe watumie fursa hii kuwaona vijana hawa wa Sukuma Flavour kwa “kuwafungulia dunia” kupitia uwekezaji wa kuwaandalia matamasha ya ndani na nje ya nchi ilikuweza kutambulika mbali zaidi kimataifa.

         Nihitimishe Makala yangu ya leo kwa kukuomba wewe msomaji wangu mpendwa upitie kwenye mtandao wa YouTube ili uweze kujionea utamu huu usioisha wa Wasukuma wa Sukuma Flavour.

          Mwandishi wa Makala haya ni mwalimu mwandamizi wa masomo ya Hisabati na Fizikia hali kadhalika ni Mbeba maono wa huduma ya Injili ya THE KING SOLOMON MINISTRY-endeleeni kubarikiwa!

          Kwa maoni au ushauri,tuwasiliane kupitia njia hizi:- +255 689-881790(WhatsApp) au mcmashamba8@gmail.com

            

Post a Comment

Previous Post Next Post

Advertising

Contact Form