Samia Suluhu Hassan! Akili Kontena! Nguvu Kisoda!

 


RAIS SAMIA SULUHU HASSAN:

AKILI KONTENA,NGUVU KISODA!

Na:Prince Ngeni Mashamba.

Habarini za leo wapenzi wasomaji wa gazeti hili la kwanza kwa ubora na ukongwe nchini Tanzania,ni matumaini yangu kuwa;nyote mu-wazima kabisa na mnaendelea vyema na majukumu yenu ya kila siku-utukufu kwa Mungu!

Katika makala haya ya leo nitakuwa nikiudurusu uongozi wa Rais Dr. Samia Suluhu Hassan pamoja na timu yake,kikubwa kilichonifanya niandike makala haya ni mtindo wake wa uongozi ambao hauna makelele mengi wa maguvu mengi katika kuyatekeleza yale ayatakayo yafanyike.Kwa ufupi ni kwamba,Rais Samia Suluhu Hassan hatumii nguvu nyingi na mikwala mingi kama wasemavyo vijana.

Mtindo wake huu wa uongozi pia,umenikumbusha msemo maarufu sana pale mitaa ya Mtoni-Kijichi kwa Wanene hadi mitaa ya Watu wa kawaida kabisa ya "Kwa Mgeninani hadi Njiapanda ya Neluka Sekondari!" Katika mitaa hii endapo mtu atakuambia, "wewe ni nguvu kontena,akili kisoda!" Maana yake wewe ni mtu unayetumia maguvu zaidi kuliko akilli katika kufanya mambo yako.Na kinyume chake humaanisha kuwa,wewe ni mtu unayetumia akili zaidi katika kufanya mambo au maamuzi yako kuliko nguvu.

Kwa mtindo na mfumo wa uongozi wa Mama Samia Suluhu Hassan ni hakika kuwa yeye ni Akili Kontena bali nguvu Kisoda.Nitajadili na kuyadadavua makala haya kwa kuzingatia vipengere mbalimbali hapa chini:

MARIDHIANO YA KITAIFA(4Rs):-Mara tu baada ya kuapishwa na kuwa Rais wa Tanzania kwa mujibu wa katiba ya nchi yetu,Rais Samia alianza kuyaponya majeraha yaliyokuwa yamesababishwa na uongozi wa mtangulizi wake Hayati John Pombe Magufuli kwa mujibu wa wadadisi wa kisiasa.Katika kulitekeleza hili,Rais Samia alikuja na kauli mbiu ya (R) nne ambazo zinasimamia maneno yafuatayo:-

Reconciliation(Maridhiano):Hapa alihakikisha kuwa pale ambapo Watanzania au Chama chake cha Mapinduzi hakikuwa kinaelewana na Wapinzani anachukua hatua za haraka kuhakikisha kuwa;maridhiano yanafanyika ili kurudisha umoja na mshikamano wa Kitaifa.

Hapa tunakumbuka jinsi alivyoamuru Mheshimiwa Freeman Mbowe na akina Esther Matiko waliokuwa wameshikiliwa katika gereza la Segerea kwa muda mrefu kuachiliwa huru kuja kuungana na familia zao.

Reformation(Kuanza Upya):Rais Samia aliamuru wale wote waliokuwa wanatuhumiwa kwa kesi za uhujumu uchumi na kesi zote zilizokuwa hazina kichwa wala miguu,nyingiwazo zilikuwa ni zile upinzai wa kisiasa;aliamuru kesi zote hizo zifutwe na waathirika waachiliwe huru.

Hapa ndipo tulipoweza kuwaona tena uraiani akina Ta-Rugemarira na wengineo wengi.

Resilience(Kuvumiliana):Hapa aliwaruhusu Watanzania wa kada zote aidha kutoka (CCM) au (ACT-Wazalendo) au (CUF) au CHADEMA kutumia haki zao kikatiba bila kuvunja amani na utulivu wa nchi yetu.Hapa ndipo tuliposhuhudia mikutano ya hadhara ikiruhusiwa na kuanza kuwasikia akina John Heche,John Pambalu na wengineo wakianza kuunguruma kwenye majukwaa ya kisiasa.

Rebuilding(Kujenga upya):Hapa alianza kujenga upya uhusiano na ushirikianao uliokuwa umepotea baina ya vyama vya Upinzani na chama Tawala.Kufuatia kazi nzuri aliyoifanya Rais Mama Samia Suluhu Hassan katika

hili hata makamu wa Rais wa Nchi ya Marekani Kamala Harris alipozuru nchini kwetu Machi 30,2023; alikuwa na haya ya kusema kumhusu Rais Samia; "Hongera sana kwa kazi nzuri unayoifanya,ninatambua kuwa umefungua milango ya kufanya kazi na vyama vya upinzani,umeondoa marufuku ya mikutano ya hadhara kwa vyama vya siasa,umeimarisha uhuru wa vyombo vya habari na umekuwa ukishiriki makongamano ya kidemokrasia!"

Zaidi sana Rais Samia aliamuru Ruzuku igawiwe sawa kwa vyama vyote vya siasa na marekebisho yafanyike kwenye muundo wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi(NEC);na mchakato wa kuandika Katiba mpya ukamilike.

KUWASHUGHULIKIA WANAMTANDAO:- Katika kuhakikisha kuwa nchi inakuwa salama,alianza kuwapangua wanamtandao wa hayati (JPM) kwa kuwateua watu wapya kabisa ambao hawakuwa wanalaumiwa kwa lolote.Hapa ndipo tuliposhuhudia akina Dotto James,Musa Samike wakipewa "big thank you" na majukumu yao kukabidhiwa kwa watu wengine.

Vilevile katika hili Tuliwashuhudia Miungu watu akina Lengai Ole Sabaya wakivuliwa madaraka yao na kuburuzwa mahakamani kujibu tuhuma za matumizi mabaya ya madaraka/vyeo vyao(Abuse of Power) yaliyokuwa yakilalamikiwa kila mahala.

KURUHUSU MIKUTANO YA HADHARA/MAANDAMANO:Toauti na ilivyokuwa kwa mtangulizi wake Hayati (JPM) ambaye alikuwa akiamini katika kufanya kazi zaidi(HAPA KAZI TU);Rais Samia aliruhusu mikutano ya hadhara kwa vyama vya upinzani na pia aliruhusu Maandamano yaliyofanywa na kuratibiwa na chama cha CHADEMA.

Siyo kwamba tu aliruhusu maandamano kufanyika bali pia aliamuru Waandamanaji hao kutoka chama cha upinzani wanalindwa na polisi wa serikali katika njia zote watakazopita,ndiyo maana siku hiyo tulishtushwa sana kumuona Mkuu wa Mkoa wa Dar-Es-Salaam ndugu Chalamila akiwapokea waandamanaji wa chama cha upinzani pasipo mabomu wala maji-washawasha;akili kontena,nguvu kisoda.

KUWATUPILIA MBALI WAHUNI/MASHETANI NDANI YA CHAMA NA SERIKALI: Katika kuhakikisha kuwa serikali na nchi kwa ujumla inaendelea kuwa salama,alianza kuwashughulikia wahuni wote(WanaCCM wanaotumia dhamana za Uongozi wao vibaya) kwa kuwatupilia mbali kutoka kwenye uongozi ndani ya Chama tawala.

Lakini hata mashetani(WanaCCM au viongozi wa serikali wanaowaza zaidi ni lini wataupata Urais kuliko kumsaidia rais aliyewateua kutekeleza majukumu na Ilani ya Chama) hakuwafumbia macho hata kidogo.Usiku wa Julai 21,2024 Rais Samia alifanya yale ambayo kwa macho ya wengi hawakuwa wanaamini kama yanaweza kufanyika;baada ya kuwatumbua mawaziri maarufu sana ndani ya Chama tawala na Serikali ya Chama cha Mapinduzi akina Nape Moses NNauye na Januari Makamba-Imeisha hiyo.

MAREKEBISHO YA SHERIA ZA UCHAGUZI:Lengo kuu la mabadiliko haya ilikuwa ni kuweka mazingira mazuri ya kisiasa nchini na kujibu kiu au shauku ya wananchi wanaotaka mabadiliko ya kisiasa.

Sheria zilizofanyiwa marekebisho(Law amendment) na Bunge ni pamoja na Sheria ya Uchaguzi wa Rais,Wabunge na Madiwani;sheria ya Tume yaa Taifa ya Uchaguzi na Sheria ya vyama vya siasa.

Nimalizie tu kwa kumtakia mitano(5) tena Rais mama Samia Suluhu Hassan na Mwenye enzi Mungu amjalie akili kontena kama Mfalme Suleimani na awatumikie Watanzania kwa Uaminifu na Uadilifu kama Mfalme Daudi.

Kwa maoni/Ushauri nicheki kupitia: +255 689 881790(WhatsAp) au +255 763 018999 au mcmashamba8@gmail,com

Mwandishi wa Makala haya ni Muinjilisti(Evangelist),Mtoa Hamasa(Motivational speaker),Mwalimu wa Sayansi(Physics/Maths),Mwandishi wa Vitabu na Makala(Author/Columnist) na Kiongozi wa biashara(Business Manager)

Post a Comment

Previous Post Next Post

Advertising

Contact Form