TUNDU LISSU:-JESHI LA MTU MMOJA LINALOLIKOSESHA USINGIZI JESHI LA WANA-CCM WENGI:
Na Prince Ngeni Mashamba.
Habarini za leo wapenzi wasomaji wa gazeti hili pendwa la Pambazuko na hususani wasomaji lialia wa makala zangu,ni matumaini yangu ya kuwa nyote mu-wazima na mnaendelea vyema na majukumu yenu ya kila siku.
Kama vile Bwana Mungu aishivyo,katika makala ya leo nitakuwa nikimdurusu kwa undani zaidi Wakili,Mwanasiasa na Mwanaharakati mahiri na mwenyekiti wa taifa wa chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania cha CHADEMA; ndugu Tundu Antiphas Mughwai Lissu aliyezaliwa katika familia ya kikulima katika kijiji cha Mahambe huko Ikungi mkoani Singida siku ya tarehe 20 Januari mwaka 1968.
Baada ya kufaulu vizuri elimu ya msingi,alijiunga na shule ya sekondari ya Ilboru iliyoko mkoani Arusha alikohitimu mwaka 1983.Alipata shahada ya kwanza ya sheria katika chuo kikuu cha Dar-Es-Salaam kati ya mwaka 1991 hadi 1994 alikohitimu na kupata shahada bora ya sheria kisha mwaka 1995 hadi 1996 alijiunga na chuo kikuu cha Warwick kilichoko nchini Uingereza kusoma shahada ya pili ya sheria.
Tundu Lissu ana mke mmoja mrembo aitwaye Alicia Magabe na watoto wake wawili waitwao Edward Bulale na Agostino Lissu.
Kabla ya kuingia rasmi kwenye siasa,Lissu aliwahi kufanya kazi ya mwanasheria wa kutetea haki ya ardhi na uhifadhi wa mazingira kwenye maeneo ya migodini; kazi aliyoifanya kwa weledi wa hali ya juu kiasi cha kuwavutia watu wengi kikiwemo chama cha siasa cha NCCR-Mageuzi alichojiunga nacho mwaka 1992 hadi 1996.
Baada ya NCCR-Mageuzi kuanza kuyumba na kukosa mwelekeo,mwaka 2004 alijiunga rasmi na chama cha Demokrasia na Maendeleo-CHADEMA ambako amedumu hadi leo hii akiwa Mwenyekiti wa taifa wa chama hicho.
Mwaka 2010 alishinda ubunge kwa kishindo na hivyo kuchaguliwa kuwa mbunge wa jimbo la Singida-Mashariki kati ya mwaka huo hadi Septemba 07,2017 aliposhambuliwa kwa risasi 38 na kunusurika kifo huku akibaki na majeraha makubwa kwenye mwili wake na risasi ambayo imekuwa ni sehemu ya mwili wake-Hakika Mungu ni mkubwa!
UANASHERIA UKO DAMUNI:-Lissu amejipatia umaarufu mkubwa kutokana na uwezo wake wa kuunda na kutoa hoja za kisheria hali inayowafanya wasomi wengi waamini kuwa sheria iko damuni na siyo mwanasheria wa vyeti tu. Hali hiyo inajidhihirisha katika matukio mengi aliyowahi kuyasimamia kama wakili na kubwa zaidi ni lile la mwaka 2017 alipoibua hoja ya ufisadi mkubwa uliokuwa umefanywa na baadhi ya viongozi wa serikali ya Tanzania almaarufu kwa jina la “The List of Shame!”
MBISHI NA MPAMBANAJI TOKA UTOTONI:-Lissu anaaminika kuwa mbishi na mdadisi tangu akiwa shule ya msingi,Sekondari hadi chuo kikuu na kubwa zaidi ni pale alipowapiga mikwala maafande wa (JKT) wakati akihudhuria mafunzo ya Jeshi la kujenga Taifa kwenye kambi ya Mafinga-JKT huko Iringa na kisha kambi ya Itende-JKT huko Mbeya.
Kutokana na mikwala ya Lissu,maafande wa Itende-JKT walifyata mkia kwa kuhisi kuwa;huenda Tundu Lissu alikuwa ni usalama wa taifa hali iliyomfanya aogopwe na kuheshimiwa.Hali hiyo ilisababisha maafande hao kuacha kumpangia zamu za kufanya kazi ngumu na badala yake akawa anapewa chakula kizuri na muda mwingi kukaa bila kufanya fatiki za kijeshi almaarufu “kula shushi!”
KWA NINI JESHI LA (CCM) LINAKOSA USINGIZI:-Kutokana na umahiri huo wa Lissu,jeshi kubwa la CCM licha ya kuwa na makomredi wengi lakini inaonekana makomredi hao hawana uwezo wa kujenga hoja za kuweza kupambana na Lissu na kijeshi chake kidogo cha Makamanda wa CHADEMA.
Wakati CCM wamekuwa wakichaguana na kupeana majukumu kambini kwao kwa kuzingatia “Uchawa Pro-max”;CHADEMA wao wamekuwa wakipangiana majukumu ya kuwakabili CCM kwa kuzingatia weledi na uwezo wa mtu katika kujenga hoja na kutekeleza majukumu.
Hivi ni kweli Mzee Stephen Masatu Wasira mwenye umri wa zaidi ya kustaafu anaweza kupambana kwa hoja na kijana kama John Wegessa Heche-jamanii huo ni zaidi ya utani.Kama Mzee Wasira aliwahi kukutwa amepiga “mbonji” yaani amelala usingizi wa pono wakati vikao vya bunge vikiendelea mjengoni je;ataweza kuendana na kasi ya utandawazi ambayo inakulazimisha kila siku uingie darasani kujifunza mamboleo-tuweni siriazi bwanaa!
Wakati hayati (JPM) alipotumiwa kama mbuzi wa kafara(scape goat/whipping boy) mwaka 2015 na hapa kazi tu, ili kukinusuru chama cha CCM kilichokuwa kimeoza kwa harufu kali ya rushwa na ufisadi kiasi cha makomredi wake kushindwa kuvaa magwanda yao ya njano na kijani kwa kuhofia kuzomewa mitaani;kwa kuwa hayati JPM hakuwa anacheka na “wowote,”kweli alifanikiwa kurudisha tena imani ya Watanzania kwa chama hicho kikongwe barani Afrika.
Baada ya hayati JPM kufariki katika mazingira yenye utata kama asemavyo Balozi Polepole,wale mafisadi papa walioikimbia nchi kipindi cha uongozi wa jembe kutoka Chato;sasa ndiyo wafadhili wakuu wa CCM na washauri wakuu wa Mwenyekiti wa CCM taifa.
CCM hii ya rais Samia imechafuka na kuwa ya hovyo kama ile ya kipindi cha rais mstaafu Jakaya Kikwete,iliyofikia hatua ya yenyewe kujivua gamba chini ya uongozi wa komredi Abdulrahaman Kinana na kijana wa Mtama Nappe Moses Nnauye;angalau kipindi hicho CCM ilikuwa bado na wazee wenye uchungu kwanza na chama chao halafu na nchi yetu lakini sasa hivi CCM imebaki kuwa ya “Wahuni” kama asemavyo Balozi Polepole.
Kingine kinachowafanya CCM kukosa usingizi,ni kuendelea kuamini kuwa Watanzania wa leo bado ni wale wa miaka ya 1970,1980,1990 wakati ambapo nchi nzima ilikuwa inasimama kwa ajili ya kuadhimisha kuzaliwa kwa CCM.Ninakumbuka miaka hiyo wakati nikiwa mwanafunzi pale shule ya Msingi Mbuye,tulikuwa tunafanya mazoezi ya nyimbo,ngonjera,maigizo hata kwa mwezi mzima tukijiandaa kumwimbia “Happy birthday to you” mtoto CCM.Ilikuwa ni lazima nchi nzima maana chama kilikuwa kimeshika hatamu,wewe ni nani hata ubishe!
CCM kinasahau kwamba sasa hivi dunia tuliyomo imekuwa kijiji(Globalized world),kwamba jambo linalofanyika Chato au Kizimkazi kwa siri tena usiku wa manane;watu walioko Mfaranyaki-Songea au Simanjiro-Manyara kwa Wahadzabe watalifahamu ndani ya sekunde chache kana kwamba nao walikuwepo wakati jambo hilo linafanyika.Kwa muktadha huo,CCM watake wasitake ni lazima waache kuchaguana na kupeana majukumu kwa kigezo cha “Uchawa pro-max” na wawakumbatie watu wenye akili za kuzaliwa na wenye uwezo wa kuchakata mambo kiutandawazi kama akina Balozi Polepole,Komredi Paul Makonda,Jaji Joseph Sinde Warioba,Mzee Joseph Butiku na Mzee Paul Mangula ambao angalau wana uwezo wa kuyajibu makombora ya makamanda wa CHADEMA.
Jambo kubwa kabisa la msingi ni kumuachia huru kamanda Lissu kwani kuendelea kumweka gerezani ni kuendelea kumpa umaarufu zaidi na hivyo kuthibitisha kabisa kuwa;CCM mnamwogopa mnoo kamanda Lissu na jeshi lake la CHADEMA lisilo na jeshi la polisi wala jeshi la ulinzi-uoga huu wa nini makomredi wenzangu wa CCM!?
Kama wakati akiwa mzima wa afya mliweza kukabiliana naye na mkamuweza inakuwaje leo muingiwe na mchecheto kiasi hicho wakati kamanda wa watu Lissu akiwa anatembea na risasi mwilini mwake!? Au CCM mmekuwa kama Goliati mbele ya kijana mdogo Daudi mwana wa Yesse-Free Lissu please!
Kama mtakwenda kufanya uchaguzi mkuu kwa kushindana na akina Luhaga Mpina,Salum Mwalimu na wagombea wengine wa kariba hiyo;mtakuwa hamjatutendea haki sisi makomredi lialia wa CCM,tutatamba vipi mtaani kama hatujamshinda Kamanda Lissu na jeshi lake la CHADEMA-tupeni raha bwanaa!
Huu utakuwa ni ushindi sawa na ule wa wale wanafunzi kutoka “Saint Kayumba” ambao huwa wanafaulu mtihani wa darasa la saba kwenda sekondari wakati hata kusoma hawafahamu-ushindi gani sasa huo!?
Nimalizie kwa kumuomba mama yetu Rais Samia na CCM kwa ujumla watupe raha kwa kutuandalia uchaguzi huru na wa haki,mnaogopa nini wakati mikutano yetu CCM inajaza maelfu ya watu almaarufu kama “nyomi la kufa mtu!”
Lakini pia msisahau kuwa jeshi la Polisi,Jeshi la ulinzi(JWTZ) na Jeshi la Fanya Fujo Uone(FFU) yote haya ni yetu;ulinzi ni asilimia 120,huo uoga unatoka wapi?
Kwa leo niishie hapa,kwa maoni au ushauri nicheki kupitia njia zifuatazo:- +255 689 881790(WhatsApp) au mcmashamba8@gmail.com