‘’KWA NINI MARAIS HAWA WA MAREKANI WALIUAWA-3??’’

 


‘’KWA NINI MARAIS HAWA WA MAREKANI WALIUAWA-3??’’

Na Ngeni Mashamba.

    Habarini za leo wapenzi wasomaji wa gazeti hili hususan wale wafuatiliaji makini wa makala haya,namshukuru Mungu kwa kutulinda na kutujalia afya njema yenye mafanikio-utukufu wote tuna mrudishia Mungu! Katika makala ya leo,ntawaletea habari  inayomhusu rais wa 25 wa nchi ya Marekani-anaitwa nani na kwa nini aliuawa?

    Rais wa ishirini na tano(25) wa Marekani anaitwa William McKinley(Mak-kinli) kama ambavyo wenyewe hulitamka jina lake,alizaliwa tarehe 29 Januari,1843 huko Niles,Ohio.Akiwa kijana mdogo,alijiunga na chuo cha Allegheny College kabla hajaanza kufanya kazi ya ualimu.Baada ya vita ya wenyewe kwa wenyewe kuanza,alijiunga na jeshi la Muungano ili kwenda kupigana vita ambako alifikia cheo cha Meja.

    Baada ya vita kuisha,alirudi kwao Ohio na kujiunga na masomo ya sheria katika chuo cha Albany Law School na baada ya kuhitimu;alifungua ofisi yake mwenyewe iliyokuwa ikitoa huduma za uanasheria.Mwaka huo huo aliamua kumwoa mwanadada aliyeitwa Ida Saxton binti wa mfanyakazi wa benki mjini hapo.Walibahatika kupata watoto wawili na mmoja wao akiitwa Katherine.Akiwa baba wa familia,alijishughulisha zaidi na shughuli za Kisiasa na Uanasheria.

    McKinley alijiingiza rasmi kwenye siasa mwaka 1869 na akaweza kupanda kisiasa kwa kasi hadi kuchaguliwa kuwa mshindi wa ugombea ubunge la Wawakilishi almaarufu kama ‘’The  U.S. Congress mnamo mwaka 1876.Kwa muda wa miaka kumi na nne(14) alikaa katika bunge la Wawakilishi na kuweza kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa kamati ya kanuni na taratibu za bunge.

    Kutokana na kuwa mtetezi mkubwa wa kuzuia kuanguka kwa uchumi wa nchi kwa kuongeza kodi katika biashara na bidhaa mbalimbali,hali hiyo ilipelekea serikali ya Marekani kuanzisha kodi iliyoitwa ‘’McKinley Tarrif’’ ikiwa ni ishara ya kumuenzi William McKinley kwa mchango wake mkubwa uliosaidia kuimarika kwa uchumi wa nchi.Kodi hiyo ilikuwa na madhara kwa maisha ya kisiasa ya McKinley kwani mwaka 1890;wapiga kura wake walimnyima kura na hivyo kulazimika kurudi nyumbani kwao Ohio alikokwenda kujipanga upya.

     Kutokana na mtikisiko mkubwa  wa uchumi uliotokea nchini Marekani hapo mwaka 1893,McKinley na wanachama wenzake wa chama  cha Republican;waliutumia mwanya huo kurudi katika ulingo wa siasa na hivyo kuweza kuwazidi kete chama kilichokuwa kinatawala wakati huo cha Democratic.

     Kutokana na uzoefu wa muda mrefu alioupata akiwa mbunge wa Congress,uwezo wake wa kutetea kudidimia kwa uchumi wa nchi na huku akiungwa mkono na tajiri maarufu wa viwanda aliyeitwa Marcus Alonzo Hanna;mwaka 1896 aliteuliwa kuwa mgombea Urais akipeperusha bendera ya  chama cha Republican.Kwenye uchaguzi mkuu alipambana na William Jennings Bryan aliyekuwa akigombea kupitia chama cha Democratic.

     Akisimamiwa kwa karibu na millionea Hanna ambaye alikuwa anaheshimika nchini humo kama mhimili wa mafanikio ya uchumi nchini Marekani,aliweza kumshinda Bryan kwa kura nyingi sana(600,000) hasa kutokana na sera zake za kihafidhina zisizopendelea mabadiliko na usawa.Ushindi huo ulikuwa ni mkubwa sana kwa chama cha Republican baada ya miaka ishirini na tano(25).

     Mara tu baada ya kuapishwa na kuwa rais wa Marekani,alipandisha kodi ya ushuru wa forodha hali iliyosaidia kupunguza kodi zingine ndogo ndogo na kutoa nafasi kubwa zaidi kwa ukuaji wa viwanda vya ndani(Domestic  industries).Hali kadhalika,mwaka 1898 aliiongoza Marekani kuipiga na kuifurusha Hispania kutoka katika koloni lake la Cuba na ilipofika Desemba,1898 mkataba wa kusitisha mapigano kati ya Marekani na Hispani ulisainiwa huko Paris-Ufaransa.Mkataba huo uliifanya Cuba kuwa taifa huru kutokana na ugandamizaji na unyonyaji wa Uhispania.Zaidi ya yote alifungua milango ya uwekezaji wa kibiashara katika nchi ya China hali iliyotoa nafasi kubwa kwa Wamarekani kuwekeza nchini China ili iendelee kuwa na nguvu katika soko la dunia.Pia mwaka 1900 McKinley alituma jeshi nchini China ili lisaidie kupambana na waasi nchini humo waliojulikana kama ‘’The Boxer Rebellion.’’

    Kutokana na sera zake za kupigania kuinua uchumi wa nchi uliofanikiwa pia kufanikiwa kushinda vita baina ya nchi yake na Uhispania,hali hiyo ilimfanya kuwa maarufu miongoni mwa Wamarekani wengi na hivyo kuweza kushinda kwa ushindi wa Tsunami katika uchaguzi mkuu uliofuata hapo mwaka 1900 huku akimshinda tena William Jennings Bryan na sera zake za kupinga ubeberu.

    Baada ya kuapishwa kwa mara ya pili kuwa rais wa Marekani hapo mwezi Machi,1901 McKinley alifanya ziara ya kuyatembelea majimbo ya Kaskazini mwa Marekani ambako kote alikopita alipokelewa kwa nderemo na vifijo.Ziara yake hiyo iliishia katika mji wa Buffalo huko New York alipowahutubia wajumbe wapatao hamsini elfu(50,000) wa mkutano uliokuwa umepewa jina la  Pan-American Exposition.

   Hata hivyo saa kumi na dakika saba(4:07pm) za jioni ya siku ya Ijumaa ya tarehe  06 Septemba,1901 akiwa katika jumba lililoitwa Temple of Music hapo hapo Buffalo,New York alipokuwa amekwenda kuhutubia mkutano wa Pan-American Exposition;alipigwa risasi mbili za tumboni na mtu aliyeitwa Leon Czolgosz ambaye baadaye alikamatwa na kufikishwa katika mikono ya sheria.Baada ya kipigo cha haja toka kwa polisi,alipandishwa kizimbani na baada ya kesi iliyoendeshwa kwa haraka-alihukumiwa kunyongwa hadi kufa hapo  tarehe 24 Septemba,1901.Mpaka leo sababu ya kwa nini Leon liamua kumuua rais McKinley inabaki kuwa kitendawili ingawa kuna hisia kuwa kulikuwa na shinikizo la kisiasa nyuma yake.

    Baada ya risasi ya kwanza kumparaza na kuja kuuawa kwa risasi ya pili,Rais McKinley alifariki dunia siku nane baadaye siku ya tarehe 14 Septemba,1901 usiku wa manane wa saa nane na robo(2:15 am).Mungu ailaze roho yake mahali pema paponi!!

     Panapo majaliwa yake Manani,tukutane wiki ijayo kwenye kona hii hii uipendayo je;itakuwa ni zamu ya rais gani na kwa nini aliuawa? Kwa maoni/ushauri tuwasiliane kwa namba  +255 689 881790 au +255 763 018999 au barua pepe ya  mcmashamba8@gmail.com          

Post a Comment

Previous Post Next Post

Advertising

Contact Form